Tundu Lissu akiongea na wafanyakazi wa Global (hawapo pichani).
Baadhi ya wafanyakazi wa Global Publishers Ltd wakimsikiliza Tundu Lissu.
Zitto atatimuliwa
MNADHIMU
Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tindu Lissu, amesema Mbunge wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe atakoma kuwa mwanachama mara tu baada ya mahakama itakapolirudisha
suala hilo chamani.
Katika mahojiano maalum ndani ya chumba cha
habari cha Global Publishers muda huu, Lissu ambaye pia ni Mwanasheria
Mkuu wa Chadema, anasema ni vigumu kwa Zitto kuendelea kuwa mwanachama
kutokana na mambo aliyoyafanya.
“Zitto alikuwa anataka uenyekiti wa chama chetu, siyo jambo baya,
lakini alishiriki kutengeneza waraka wa siri, siri kubwa, ambao
haukubaliki. Alimtuhumu mwenyekiti wetu kuwa hana elimu, malaya, mnunuzi
mkuu wa mali za chama, fisadi na mambo mengine mengi ya namna hiyo. Huu
ni uongo mkubwa, hatuwezi kuukubali.
“Ni vigumu kuzungumzia umalaya wa mwenyekiti wetu lakini nadhani hayo
ni mambo ya chumbani ambayo kwa vyovyote huwezi kuyaunganisha na
uongozi. Hayo ni mambo binafsi, kama tungekuwa tunalinganisha mambo
hayo, sijui tungesema nini kuhusu Rais Nelson Mandela na Bill Clinton wa
Marekani ambaye alikumbwa na kashfa katika mojawapo ya vibaraza vya
Ikulu ya White House,” alisema.
Lissu alisema Zitto, akiwa Naibu
Katibu Mkuu, anafahamu kuwa kila jambo linajadiliwa na Kamati Kuu ambayo
yeye ni mjumbe na kwamba tuhuma zote dhidi ya Mwenyekiti na Katibu Mkuu
ni uongo.
Kuhusu ukomo wa nafasi ya Uenyekiti wa Chadema Taifa, alisema waraka
wa mabadiliko ya katiba ulitolewa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu mwaka
2006, Shaibu Akwilombe aliousambaza kwa wenyeviti wa Wilaya na Mikoa
Tanzania nzima uliowataka kuridhia kuondoa kipengele cha ukomo wa nafasi
hizo, vinginevyo chama hicho kingekufa kwa vile kusingekuwa na kiongozi
halali hadi wakati huo.
“Chama chetu kilitaka kuondoa ukomo huo kwa sababu awali, kilisema
kila baada ya miaka kumi viongozi wangetoka, lakini baada ya kulitazama
kwa makini, tukagundua kwamba tungekuwa hatuna viongozi kama
tungeendelea na utaratibu ule kwa sababu ingefikia baada ya miaka kumi,
viongozi wote wanatoka, sijaona chama hicho kama kipo hapa nchini,”
alisema Lissu.
Yeye ni msumbufu bungeni?
Kuhusu kuonekana kama yeye ni mtu wa vurugu bungeni, Lissu alisema
siyo kweli, bali ni mtu mwenye kusimamia kanuni na ndiyo maana
anaonekana kuwa hivyo.
Alisema kilichopo hivi sasa ni kuwa ndani ya Bunge la Kumi kuna
wabunge wengi wajuaji wameingia (sio wajuaji kama tunavyosema
uswahilini, ni wajuaji kwa maana ya wajuaji hasa wa mambo).
Alisema
wanajua kutafsiri kanuni na wanazisimamia. “Nadhani ni bunge hili ndilo
wananchi wamejua baadhi ya lugha za bunge kama Mwongozo wa Spika na
kadhalika, wananiona nina vurugu kwa sababu ninasimamia ukweli.
“Katika Rasimu hii ya Katiba, kumefanyika mabadiliko mara tatu,
wanaongea wanakubaliana, lakini baadaye mimi ninasimama na kusema
tatizo. Na nikuambie, hoja zote zilizosababisha kufanyiwa kwa
marekebisho katika mara zote tatu, zilianza kwenye mkoba wangu, kwenye
kalamu yangu, maoni yote kuhusu katiba niliyaanzisha mimi na kuyafanya
kuwa ya kambi rasmi ya upinzani bungeni,” alisema Lissu.
Alisema Rais
Jakaya Kikwete amekuwa akimshambulia kwa kumuita kama mwanasheria
msumbufu, lakini kwake ni fahari kwa sababu wakati anamsema hivyo, pia
mapendekezo yake yamekuwa yakifanyiwa kazi kila mara.
Samuel Sitta na Anne Makinda nani zaidi?
Akizungumzia
kuhusu bunge lililokuwa chini ya Spika Samuel Sitta na wa sasa, Anne
Makinda, Lissu alisema enzi za Sitta bunge kama taasisi, lilikuwa na
nguvu na lenye hadhi, lakini hili la sasa, spika amekuwa akilitumia kwa
ajili ya kuitetea na kuilinda serikali badala ya kuisimamia na
kuiwajibisha.
Alisema endapo bunge lililo chini ya Mama Anne Makinda
lingekuwa linaendeshwa kwa manufaa ya wananchi, mambo mengi makubwa
yangetokea, kwani kuna madudu mengi sana yaliyofanyika kuliko hata
kipindi cha Sitta.
“Chukulia Operesheni Tokomeza Ujangili kwa mfano. Kama mambo
yengekwenda sawa, serikali nzima ingewajibika, tofauti na sasa
tunapoambiwa mawaziri wanne tu wamejiuzulu.
“Ile ilikuwa ni operesheni ya kijeshi, ni kama jeshi lilikuwa vitani.
Ni nani anatangaza vita? Ni Rais, lakini pia rais kabla ya kuliingiza
jeshi vitani, ni lazima tamko hilo lije bungeni lijadiliwe, hatujaletewa
bungeni kulijadili, lakini jeshi limeingia vitani dhidi ya raia,
wameuawa Watanzania wengi sana, wengi wamejeruhiwa, wengine kupata
vilema vya maisha.
“Kama ripoti ya kamati ya Lembeli ingejadiliwa kwa uwazi, serikali
nzima ingewajibika. Hii yote ilitokana na utendaji usioridhisha wa spika
wetu wa sasa, Anna Makinda,” alisema.
Soma zaidi alichokisema Lissu katika Magazeti ya Global Publishers…..
0 comments:
Post a Comment