Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania – TRL unawatangazia abiria
wote na wananchi kwa jumla kuwa kutokana na sababu za kiufundi
unasikitika kuwa treni ya abiria iliyopangwa kuondoka leo Jumanne
Januari 07, 2014 saa 3 usiku kwenda bara imeahirishwa hadi
keshokuwa siku ya Alhamis Januari 09, 2014, saa 3 usiku.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa dharura hiyo ya kuahirisha safari
imetokana na ajali ya treni ya mizigo iliyotokea juzi saa 2 usiku kati ya
Stesheni za Luiche na Kigoma na kusababisha treni ya abiria kutoka
Kigoma kushindwa kuondoka kuja Dar.
Wakati huo huo taarifa iiliyopatikana mchana huu imethibitisha kuwa
ukarabati wa eneo lililoathirika na ajali ya treni ya mzigo ya juzi
umekamilika na njia imefunguliwa saa 8:45 mchana huu. Aidha treni
ya abiria kutoka Kigoma kuja Dar imeshaondoka mjini Kigoma tokea
saa 9:20 alasiri ya leo.
Aidha taarifa hii iwafikie wadau wote wa usafiri na huduma ya reli
ya kati na kwamba uongozi wa TRL unaomba radhi kwa usumbufu
wowote utakaojitokeza.
Imetolewa na Ofisi ya Uhusiano kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji
Mhandisi Kipallo Amani Kisamfu.
TRL Makao Makuu,
Dar es Salaam.
Januari 07, 2014
0 comments:
Post a Comment