Bw John Collenette wa ACE Africa
Afisa Balozi -Minister Counsellor- Amos Msanjila akizungumza na Freddy Macha na Urban Pulse.
Amos Msanjila, Tom Pearson, Dilip Navapurkar, Balozi Kallaghe, Ali Lyon, Nicolas Zafiriou, Glen Pierce, Yusuf Kashangwa.
Balozi Kallaghe na msafara. Kulia kwake ni Bw Dilip Navapurkar na mwanzo Kocha Glen Pierce-picha na Urban Pulse.
Balozi na wageni wote. Kwanza kabisa kulia ni Mkurugenzi wa Biashara Ubalozini, Yusuf Kashangwa-Pic by Urban Pulse.
*****
*****
Picha na Urban Pulse
Imeandikwa na Freddy Macha
Mradi wa majaribio ya mwezi mmoja ulioandaliwa na Waingereza kuendeleza shule sita
wilaya za Arusha na Moshi unatazamiwa kuanza wiki hii, ilitangazwa London, mwishoni
mwa juma.
Mradi huu unaosimamiwa na kampuni ya kitalii, Safari Hub na Chuo cha Eton
wakisaidiana na Ubalozi wa Tanzania, Uingereza, unatuma Mkuu wa Mafunzo ya
Michezo Eton, Bwana Glen Pierce na wanafunzi watatu waliomaliza kidato cha sita
wanaotarajia kuingia vyuo vikuu baadaye mwakani.
Nchini shughuli hii itasaidiwa na ushirikiano wa chuo cha michezo Arusha (Future Stars
Academy) na shirika la ufadhili linalopigana kuondoa umaskini, (ACE Africa).
Akiongea katika tafrija ndogo iliyofanywa Ubalozini, London kuuaga msafara ,
Mkurugenzi Mkuu wa Safari Hub, bwana Dilip Navapurkar alisema iko haja ya kujenga
ujuzi toka utotoni ili “kuhakikisha timu ya taifa ya Tanzania inafanya vizuri katika
michuano ya Kombe la Afrika na Dunia na kufikia kiwango cha mafanikio tunayoyaona
nchi nyingine mathalan Nigeria, Ghana, Afrika Kusini na Ivort Coast.”
Mwalimu Pierce mwenye uzoefu wa Miaka 27 chuo cha Eton aliwafundisha pia wajukuu
wa Malkia Uingereza, William na Harry. Wanafunzi atakaoongozana nao ni Tom
Pearson, 18 ( ulinzi) Nicholas Zafiriou, 18 (kiungo) na Ali Lyon, 19 (mshambuliaji
). Wamechaguliwa kwa kufanya vizuri katika michezo mbalimbali ukiwemo mpira
waliocheza timu ya shule ya Eton.
Eton ilianzishwa karne ya 15 na Mfalme Henry wa 6 na ni moja ya shule bora sana
duniani. Mawaziri Wakuu 19 wa Uingereza (akiwemo Winston Churchill, Tony Blair,
David Cameron na Meya wa Jiji la London, Boris Johnson) walisoma hapa. Wabunge,
mawaziri, waandishi maarufu (George Orwell na Ian Fleming mtunzi wa visa vya James
Bond) na watoto wa wafalme mbalimbali duniani vile vile wamesoma Eton.
Tafrija ya kuwaaga ilifanywa na Balozi Peter Kallaghe na Afisa Balozi, Amos Msanjila
aliyewakaribisha Tanzania. Mbali na kutoa mafunzo ya michezo wageni wanatazamiwa
kukutana na wanahabari Jumanne, kutembelea mbuga za wanyama, Zanzibar na
kupanda mlima Meru, Arusha.
Lengo la mradi huu ni safari au mradi mfupi na hatimaye kuendeleza mahusiano kati
ya wanafunzi wa Tanzania na Eton. Iko siku “timu ya mpira ya Eton itafanya ziara
Tanzania na hatimaye Watanzania pia kuitembelea Eton,” Bwana Navapurkar alisema.
Akihimiza umuhimu wa safari hii, Balozi Kallaghe aliwaambia wageni kwamba
Watanzania wanapenda sana soka na kuwaahidi wageni kuwa watafaidi uzuri wa nchi
watakapofika kama sehemu ya mafanikio ya kibiashara siku za mbeleni na kufurahia
michezo Tanzania.
Akijibu maswali ya wanahabari, Bwana Navapurkar alisema gharama za safari na vifaa
vimetokana na michango ya watu binafsi na shule zinazopakana na Eton ambazo
zimefikia shilingi milioni 61 na nusu.
Mbali na mafunzo ya mpira wanafunzi Arusha na Moshi watapewa vifaa na kufundishwa
maana ya nidhamu, elimu na michezo, aliongeza kocha Glen Pierce. “Watoto
watakaopewa fursa hiyo ni wale tu watakaohudhuria shule,” alisisitiza.
Akisifia tabia ya Watanzania, Mkurugenzi wa Safari Hub, yenye makao Tanzania,
Bwana Navapurkar, alisema Tanzania imechaguliwa shauri ni nchi yenye amani,
demokrasia na utulivu wa kisiasa, ukilinganisha na nchi nyingine za Kiafrika. “Tanzania
ni kito cha maendeleo ya Afrika.” Alisema.
0 comments:
Post a Comment