Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mh.Freeman Mbowe.
Kama
mojawapo ya mikakati ya baadhi ya watu wanaotaka kuhamisha mjadala wa
makosa yanayowaandama ya utovu wa maadili na usaliti dhidi ya chama,
hivi karibuni, Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe amezushiwa
tuhuma zisizokuwa na ukweli wowote zikilenga kumchafua kwa nafasi yake
ya uongozi na kuipaka matope taasisi anayoiongoza;
Tuhuma hizo ni pamoja na;
1.
Kwamba Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa mwaka 2005 eti alichukua fedha kutoka
kwa Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono kiasi cha sh.Milioni
40 ili Mwenyekiti Mbowe asifanye kampeni katika jimbo hilo.
2.
Mwaka 2008, eti Mbunge Mkono alimpatia Mwenyekiti wa Chama Taifa, sh.
Milioni 20 kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa Tarime, kisha akazitoa kwenye
chama kama mkopo na akalipwa.
3.
Mwaka 2010, wakati wa uchaguzi mkuu Mbunge Mkono eti alimpatia
Mwenyekiti wa Chama Taifa sh. Milioni 200 kwa ajili ya kampeni za
mgombea urais.
4.
Mwaka huo huo wakati wa uchaguzi mkuu, eti Mwenyekiti wa Chama Taifa,
alipokea sh. Milioni 100 kutoka kwa Rostam Aziz kwa ajili ya kampeni.
Idara ya Habari ya CHADEMA, inapenda kusema yafuatayo;
1. Hakuna
ukweli hata mmoja katika tuhuma hizo. Ni uongo na uzushi uliopangiliwa
kama moja ya mikakati ya watu wenye malengo ya kutaka kuilaghai jamii
kwamba viongozi wa CHADEMA hawana tofauti na wale wa CCM na kwamba chama
hiki kikuu cha upinzani kinachobeba matumaini ya Watanzania katika
kupigania haki zao na kupinga kila aina ya ufisadi, kionekane hakina
tofauti na chama kilichoko madarakani, ambacho kimepoteza ushawishi kwa
wananchi.
2. Matokeo ya uongo huo ni kutaka kuisaidia CCM na kugeuza mjadala.
3.
Idara ya Habari ya CHADEMA inapenda kuuambia umma wa Watanzania wote,
hususan wanachama, wapenzi, mashabiki wa CHADEMA na wapenda mabadiliko
nchini kwamba,Mwenyekiti wa Chama Taifa, ameshawasiliana na mawakili
walifanyie kazi suala hili kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria.
4.
Kwa uhakika tunapenda kuiambia jamii ya Watanzania wote, hususan
wanachama, wapenzi, mashabiki wa CHADEMA na wapenda mabadiliko wote
nchini, kwamba; Chama wala Mwenyekiti wa Chama Taifa, mahali popote na
wakati wowote, hajawahi kupokea msaada wa fedha hizo kutoka kwa
waliotajwa kwa malengo yaliyosemwa.
5.
Tungependa kuwaambia waliozusha tuhuma hizo, ni vyema kama wanapenda
kutunza heshima kidogo waliyobakiza katika jamii kutokana na kuelemewa
na mzigo wa tuhuma za utovu wa maadili na usaliti dhidi ya CHADEMA,
badala ya kugeuka kuwa mabingwa wa kupika uongo, wajibu masuala ya
msingi yanayowaandamana kuhusu mikakati yao ya kuhujumu CHADEMA na
viongozi wake, ambayo iwapo chama kisingeibaini na kuchukua hatua za
kinidhamu, ingesababisha kuua ndoto na matumaini ya Watanzania kufanya
mabadiliko ya kimfumo na kiutawala, kwa kuiondoa CCM madarakani.
6
Taarifa kuhusu baadhi ya tuhuma katika mkakati huo ambazo zimemlenga
Mwenyekiti wa Chama Taifa, kwa kuhusisha shughuli zake binafsi za
uwekezaji, zitajibiwa kupitia taasisi husika.
Tumaini Makene
Ofisa Mwandamizi wa Habari- CHADEMA
0 comments:
Post a Comment