Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya mwaka 2013 ambayo hutolewa kila mwaka na Shirika la Afya Duniani, Balozi aliwaeleza wageni waalikwa katika hafla hiyo kwamba ushiriki wa viongozi wa afrika kupitia mtandao wao wa ALMA umechangia sana katika kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na Malaria.
Dkt. Robert Newman kutoka WHO yeye amesema, inasikitisha pale inapobidi mtoto apoteze maisha kwa sababu tu ameshindwa kupatiwa chandarua ambayo thamani yake ni dola tano. amewataka viongozi na washirika mbalimbali kutobweteka na mafanikio katika kuudhibiti ugonjwa huo mafanikio nayohusu kupungua kwa maambukizo ya ugonjwa wa malaria na vifo vya watoto chini ya miaka mitano.
Bw, Ray Chambers ambaye ni Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema inatia moyo sana kuona vitanda katika wadi za watoto vikiwa vitupu mahali ambapo watoto walikuwa wakilala wawili katika kitanda kimoja kutokana na kusumbuliwa na malaria.
Dkt. Fatoumata Traore ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa Roll Back Maralia akizungumza wakati wa halfa hiyo.
Na Mwandishi Maalum
Utashi wa kisiasa unaoonyeshwa na marais wa Afrika katika kudhibiti ugonjwa wa malaria, pamoja na ushiriki wa wadau mbalimbali akiwamo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon umeanza kuzaa matunda kufuatia taarifa za kutia matumaini zinazoonyesha kupungua kwa vifo vitokanavyo na ugonjwa wa malaria.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya mwaka 2013 ya Shirika la Afya la Dunia ( WHO ) kuhusu mwelekeo wa ugonjwa wa malaria katika kipindi hicho , Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi amesema hapana shaka kwamba mwamko ulioonyeshwa na Marais wa Afrika kupitia muungano wao dhidi ya Malaria ( ALMA) umechangia kwa kiasi kikubwa.
Jana Alhamis Bw. Ray Chambers ambaye ni mjumbe maalum wa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Malaria kwa pamoja na Dkt. Robert Newman ambaye ni Mkurugenzi wa mradi wa Malaria (WHO), Bi. Fatoumata Traore Mkurugenzi Mtendaji wa Roll Back Malaria na Bi. Joy Phumapi ambaye ni Katibu Mtendaji wa ALMA walizindua ripoti hiyo mbele ya Wawakilishi wa Kudumu wa Nchi za Afrika na wadau wadau wengine.
Akiwakaribisha wageni waalikwa kwa niaba ya Balozi wa Msumbiji katika hafla hiyo iliyoandaliwa na ALMA, Balozi Manongi alisema ripoti za kila mwaka za WHO zimekuwa zikionyesha mwelekeo mzuri katika kuushughulikia ugonjwa huo ambao unaadhiri kwa kiasi kikubwa watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano. Na kusisitiza kwamba Afrika inatakiwa kuzitumia ripoti hizo kuongeza kasi katika kuikabili Malaria.
“Ripoti hizi zinaonyesha kwamba tukishirikiana tunaweza kabisa kuidhibiti malaria, viongozi wetu wameonyesha mfano kwa kuanzisha muungano wao dhidi ya malaria, ni wajibu wetu kuendelea kukusanya nguvu na kujituma Zaidi ili tusirudi nyuma” akasisitiza Balozi Manongi.
Ripoti ya malaria kwa mwaka huu, ambayo ni mkusanyiko wa taarifa kutoka nchi 102 zikiwamo 10 ambazo zimeathirika sana na ugonjwa wa malaria na taarifa kutoka vyanzo vingine, inatoa tathmini ambayo pamoja na mambo mengi kwamba onyesha ushirikiano kati ya serikali, mashirika ya kimataifa na wafadhili umewezesha katika kipindi cha mwaka 2000-2012 kuokoa maisha ya watu 3.3 milioni ambayo yangepotea kutoka na ugonjwa huo.
Taarifa hiyo inaeleza Zaidi kwamba ugonjwa wa malaria umepungua kwa asilimia 45 duniani kote na kwa asilimia 49 katika nchi za Afrika zinazohudumiwa na WHO.
Akizungumza katika uzinduzi huo Dkt. Robert Newman kutoka WHO amewaeleza Mabalozi kwamba ripoti inahabari njema kuwa ugonjwa wa malaria umepungua kwa kiasi kikubwa sana katika kipindi hicho cha kati ya 2000-2012.
“ kuna punguzo la asilimia 54 la vifo vya watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano vitokanavyo na malaria katika nchi za afrika hususani zile ambazo zimeathirika Zaidi.
Takwimu hizi na nyingine zilizomo katika ripoti hii zinathihirisha wazi kwamba tukishirikiana tunaweza kuleta mabadiliko makubwa katika kuikabili Malaria” akasema Dkt Newman Akaongeza kwamba licha utashi wa kisiasa ulioonyeshwa na viongozi mbalimbali kumekuwapo na mwitikio unaoridhisha wa uchangiaji wa raslimali fedha katika eneo hilo. Ambapo katika kipindi hicho jumla ya dola za kimarekani bilioni mbili zilitolewa na wafadhili na dola milioni mia tano zilitolewa na nchi ambazo zimeathirika Zaidi.
Hata hivyo akasema ingawa mwamko wa kuchangia umekuwa mkubwa bado lengo halijafikiwa la kiasi cha dola za kimarekani 5.1 na kuonya kwamba bado michango inahitaji na wala mafanikio hayo yaliyopatikana yasijewafanya wadau wakabweteka kuchangia au kuhamishia fedha kwenye masuala mengine.
“ hatupashwi kubweteka au kuridhika na mafanikio haya, haipendezi mtoto au mtu kufariki kwa sababu tu ya kushindwa kuwa na uwezo wa kununua chandarua ambayo thamani yake ni sawa na dola tano ya kimarekani. Na weza kusema mafaniko haya ni sawa na nusu glasi. Hebu pata picha kama wewe ungekuwa ni mtoto unayeishi katika maeneo ambayo yameathirika vibaya na malaria halafu hakuna hata dawa za kukutibu, bila shaka matarajio yako ni kuona glasi imejaa na si nusu glasi au glasi iliyotupu” akasisitiza Muwakilishi huyo wa WHO.
Naye Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Malaria na ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuchagiza na kutafuta raslimali zikiwamo fedha kwaajili ya miradi ya malaria, Bw. Ray Chambers alikuwa na haya ya kusema.
“Ripoti hii ya WHO inatoa matumaini sana, ukizingatia kwamba katika miaka iliyopita takribani watoto milioni moja walikuwa wakipoteza maisha kwa malaria leo hii idadi hiyo imepungua hadi kufika nusu ni jambo la kutia faraja sana” akasema Chembers.
Na kuongeza. “ nimetumia muda mwingi Afrika nimeshuhudia watoto wakifariki, nimejionea wadi za watoto zilivyokuwa zimejaa huku watoto wakilala wawili katika kitanda kimoja. Lakini leo hii katika baadhi ya nchi wadi za watoto zipo tupu na vitanda vinatumika kwa huduma nyingine”.
0 comments:
Post a Comment