Azam
Media Limited imefanikiwa kukamilisha utaratibu wa ushirikiano na
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) utakaowawezesha mashabiki wa
kandanda kote nchini kunufaika kwa kuona michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom
kila mwishoni mwa juma hadi kukamilika kwa nusu ya msimu wa 2013/14
kupitia TBC1 kwa hisani ya AzamTV.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi (Kamati ya Ligi) wameeleza kuunga mkono utaratibu huu makini.
“Baada
ya kupata haki za matangazo ya luninga ya Ligi Kuu ya Vodacom, moja ya
shabaha zetu kuu imekuwa ni kuhakikisha kuwa tunafanikiwa kurusha
matangazo yanayokidhi viwango vya kimataifa kwa ubora. Ili kufanikisha
shabaha hiyo tumewekeza vilivyo katika teknolojia ya kisasa ya vifaa vya
matangazo ya nje (Outside Broadcasting) na katika mafunzo kwa watumiaji
wa vifaa hivyo. Ninayo furaha kusema kuwa matayarisho yamekwenda vema
kiasi kwamba tumejikuta tuko tayari kurusha matangazo ya kiwango cha juu
kabla hata ya kuzinduliwa kwa huduma kamili za AzamTV”, alisema Rhys
Torrington, Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media Limited.
“Kwa
kuwa mashabiki wengi kote nchini wanangojea kwa hamu kubwa kuziona timu
wazipendazo, imeonekana ni vema kuanza kuonesha michezo hii ya Ligi
sasa. Kwa kuzingatia hali hiyo, nilifanya mazungumzo na rafiki zetu pale
TBC na kuwaomba iwapo wana uwezo na kuridhia kurusha matangazo yetu ya
moja kwa moja bila ya malipo yoyote kuanzia mwisho wa juma hili hadi
kukamilika kwa nusu msimu. Tulifanikiwa kufikia makubaliano kwa haraka
na sasa tunafanyia kazi masuala ya kiufundi yatakayowezesha kuwa tayari
kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi utakaofanyika Uwanja wa Taifa”,
Aliongeza Bw. Torrington.
Mara
tu huduma kamili za AzamTV zitakapozinduliwa majuma machache yajayo,
matangazo ya michezo ya Ligi Kuu kwa wigo mpana yatakuwepo pia kwenye
chaneli yake hadi mapumziko ya nusu msimu. Baada ya hapo matangazo ya
Ligi Kuu ya Vodacom yatapatikana kwa wale tu watakaokuwa na visimbuzi
(decorders) vya AzamTV.
0 comments:
Post a Comment