SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Wednesday, June 22, 2011

WAKE WA VIONGOZI WA AFRIKA WATAKIWA KUSHIRIKIANA ILI KUHAKIKISHA KUWA MATATIZO YANAYOWAKABILI KINAMAMA NA WATOTO YANAPATA UFUMBUZI

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiongea katika hafla ya chai ya jioni iliyoandaliwa na Mke wa Waziri Mkuu wa Malaysia Datin Paduka Seri Rosmah Mansor maaulum kwa wake wa viongozi nyumbani kwake Putrajaya Malaysia.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete (kushoto ) akiongea na baadhi ya wake wa viongozi wa kitaifa kutoka nchi za Afrika wakati walipokaribishwa kwenye hafla ya chai ya jioni na mke wa Waziri Mkuu wa Malaysia Datin Paduka Seri Rosmah Mansor (kulia) nyumbani kwake Putrajaya Malaysia. (.Pichani akifuatiwa wa pili kulia) ni Mke wa Makamu wa Rais wa Kenya Mama Pailine Kalonzo pamoja na mke wa Waziri Mkuu wa Lesotho Mama Mathato Mosisili (wa tatu kutoka kulia).
Baadhi ya wageni waalikwa wakiwa katika hafla hiyo.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete pia Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA (kushoto) wakibadilishana mawazo Juni 22,2011 na mke wa Waziri Mkuu wa Lesotho Mama Mathato Mosisili (nguo ya mistari) pamoja na mwenyeji wao Mke wa Waziri Mkuu wa Malaysia Datin Paduka Seri Rosmah Mansor (kulia) nyumbani kwake Putrajaya Malaysia. alipowaalika kwenye chai ya jioni.(Picha na Mwanakombo Jumaa-MAELEZO).
*****************************
Na Anna Nkinda – Putrajaya, Malaysia.
Wake wa viongozi wa Afrika wameshauriwa kutunza mahusiano yaliyopo baina yao ili waweze kushirikiana kwa pamoja kutatua matatizo yanayowakabili wanawake na watoto katika nchi zao kwani kundi hili limesahaulika kwa kiasi kikubwa katika jamii.
Ushauri huo umetolewa jana na Mke wa Waziri Mkuu wa Malaysia  Mama Datin Paduka Seri Rosmah Mansor alipokuwa akiongea na wake wa viongozi kutoka nchi za Tanzania, Lesotho, Kenya na Zambia wakati walipomtembelea nyumbani kwake Putrajaya kwa ajili hafla ya chai ya jioni.
Alisema kuwa moja ya malengo ya kazi zao ni kuhakikisha kuwa kina mama na watoto wanaishi katika mazingira salama hivyo basi kama wanataka kufanikiwa zaidi jambo la muhimu ni kufanya kazi kwa pamoja na kubadilishana  mawazo waliyonayo kwani Afrika ni moja na changamoto zinazowakabili wanawake na watoto zinafanana.
“Kazi mnazozifanya zinafanana na kuna malengo ambayo mmejiwekea ili muweze kufanikisha kazi zenu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa kina mama na watoto wanaishi katika mazingira salama hivyo basi ni lazima muungane na kuwa kitu kimoja hakika kwa kufanya hivi mtaweza kumkomboa mwanamke na mtoto wa kiafrika”, alisema Mama Mansor.
Mama Mansor aliendelea kusema kuwa kutokana na uhalisia ni rahisi kwa wanaume kujiangalia wao wenyewe na kutatua matatizo yao lakini kwa wanawake na watoto wanatakiwa kupewa uangalizi wa ziada na msaada wa lazima hasa kwa wale wanatoka katika familia maskini.
Akiongea kwa niaba ya wenzake Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alisema kuwa wao kama wake wa viongozi wanakazi kubwa ya kuhakikisha kuwa kinamama na watoto wanapata huduma muhimu katika jamii ikiwa ni pamoja na elimu na afya.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa kwa upande wa Tanzania amekuwa akijitahidi kuhakikisha kuwa watoto wa kike ambao ni yatima wanapata elimu na vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinapungua.
“Taasisi yangu ya WAMA imesaidia katika jitihada za Serikali kuhakikisha kuwa vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinapungua kwa kuchangia  vifaa vya afya katika Hospitali, vituo vya Afya na Zahanati na kutoa elimu kwa jamii kupitia kampeni mbalimbali za uhamasishaji”, alisema Mama Kikwete.

0 comments:

Post a Comment