SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Wednesday, October 13, 2010

Yanga saa 48 gizani Mwanza



Na Erasto Stanslaus
KLABU ya soka ya Yanga, kesho Alihamisi inatarajia kuifuata Simba jijini Mwanza huku ikiwa imemaliza maandalizi ya kuwaua wapinzani wao hao wa jadi katika mchezo wao utakaochezwa Jumamosi, Oktoba 16 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Yanga ambayo iliweka kambi wilayani Bagamoyo, Pwani kujiandaa kwa mchezo huo, itatua Mwanza kesho ikiwa na kikosi chake kamili ambacho kimeiva kwa mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom na wamepanga kutua mkoani humo kimya kimya na kujichimbia kusikojulikana kwa saa 48 hadi Jumamosi ambayo ndiyo siku ya mchezo.
Msemaji wa klabu hiyo, Louis Sendeu aliliambia Championi Jumatano, kuwa wapo tayari kwa mpambano huo na wanatarajia kuibuka na ushindi mnono kutokana na maandalizi kabambe waliyofanya.
“Tunashukuru Mungu kikosi kipo vizuri hakuna mchezaji yeyote ambaye anaweza kukosa mchezo huo, hivyo tunaamini tutaibuka na ushindi mnono kutokana na maandalizi mazuri tuliyofanya,” alisema Sendeu.
Kwa upande wake kocha mkuu wa kikosi hicho, Kosta Papic, alisema: “Nimemaliza kazi ya kuiua Simba, hivyo sina wasiwasi juu ya ushindi katika mchezo huo na wachezaji wote wapo vizuri.”
Yanga itaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mchezo wa Ngao ya Jamii kwa njia ya penalti 3-1, lakini kazi itakuwa ni katika kulipa kisasi cha kufungwa michezo yote miwili ya Ligi Kuu ya Vodacom msimu uliopita

0 comments:

Post a Comment