SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Friday, May 7, 2010

Shivji atema cheche

*Adai WEF ni kuendeleza ubeberu
Na Job Ndomba
  MAANDAMANO ya wanaharakati yaliyotakiwa kufanyika jana na kuishia katika Viwanja vya Mlimani city kunakofanyika mkutano wa Jukwaa la Uchumi la Dunia kwa Afrika (WEF) yamefanyika kwa namna yake ambapo yalianzia ndani ya Ofisi za Mtandao wa Jinsia Tanzania (TNGP) na kuishia nje ya viwanja vya ofisi hizo, huku Profesa Issa Shivji akimwaga 'cheche' akidai kuwa mkutano wa WEF ni wa kuendeleza ubeberu wa kibepari.
  Hayo yalitokea jana wakati wa jukwaa la wananchi wa Afrika liliandaliwa na wanaharakati hao ili lifanyike sambamba na Jukwaa la Uchumi la Dunia kwa Afrika linaloendelea Jijini Dar es Salaam kuanzia jana.
Akizungumza katika Jukwaa hilo, Prof. Shivji alisema kuwa mkutano huo wa WEF hauna faida ya kimaendeleo kwa Afrika zaidi ya kuendeleza mfumo wa kibepari unaoendelea kunyonya nguvu na raslimali za waafrika.
  "Kwa ujumla mkutano huo hauna faida kabisa kwetu zaidi ya kuendeleza mikakati ya kibeberu na kibepari ya kuwanyonya Waafrika," alisema Prof. Shivji.
  Prof. Shivji alisema mkutano huo ni wa wababe wanaojiita CEOs wa makampuni ya kimataifa na makampuni ya kibepari na mashirika ya kimataifa kama benki ya dunia ambao wamejichukulia hatua ya kujadili hatma ya wengi, bila ya wao kusikilizwa na ndani yao kuna wapambe wasomi wanaotetea mfumo wao wa kibepari.
  "Ukweli wa mkutano huo ni kwamba, ni wa uchumi wa kibeberu na kibepari na watu wa Afrika hawana budi kuelewa kwa undani na kwa ufasaha mfumo huo ambao unatawala duniani na kusimamiwa na hao wanaokutana kule Mlimani City.
  "Hatuwezi kuzungumzia ukombozi wa mnyonge na wazalishaji wadogo bila kuelewa mfumo huo ambao kihistoria na sura yake mpya ni ubepari mamboleo na sababu waafrika tunaguswa moja kwa moja na mfumo huo," alisema.
  Alisema mfumo huo ni unyang'anyi unaolindwa na sheria iliyowekwa na wenyewe na kwa Afrika kumekuwa na mfumo huo kwa karne tano.
  Prof. Shivji alisema kutokana na mifumo kama hiyo kumekuwa na mpasuko wa kitabaka ambao umeonekana kukua na kuwa na matabaka mawili katika taifa moja, yaani waliokuwa nacho na wasiokuwa nacho.
  "Mwenyezi Mungu hakuumba matajiri kwa upande mmoja na maskini kwa upande mwingine, wala mabepari kwa upande mmoja na wafuta jasho kwa upande mwingine, hayo ni matokeo ya kihistoria," alisema.
Aliongeza kuwa ukweli ni kwamba ubepari leo hauhitaji Waafrika bali unahitaji Afrika na kwamba hawana haja ya watu bali wanahitaji vitu, rasilimali na ardhi.
  Akizungumzia suala la maandamano alisema kuyazuia ni kuwanyima watu haki ya msingi ya kutakiwa kutoa sauti zao ili ziweze kusikika.
  Hata hivyo, licha ya maandamano hayo kuanza na kuishia katika eneo hilo la umbali mfupi lakini yalikuwa na mbwembwe za aina yake huku yakiongozwa na mabango yaliyokuwa yamesheheni ujumbe wa aina mbalimbali.
  Mbwembwe hizo ni pamoja na kuwa na kuongozwa na sanamu lilikuwa limevalia kanzu kubwa lenye maandishi 'Viongozi wa Afrika ni wazalendo au vibaraka'.
  Aidha mabango mengine yalikuwa yakisomeka 'Ubinafsishaji ni ukoloni mamboleo', 'wawekezaji hawatufai waondoke', 'Vita barani Afrika ni mbinu za kuchota rasilimali zetu', na 'wanawake ni wakuzaji wa uchumi katika jamii'.
  Awali akifungua mkutano wa Jukwaa hilo mbadala, Mkurugenzi wa Action Aid International Tanzania, Bi. Aida Kiangi alisema  lengo kubwa la jukwaa hilo ni kujadili kwa mapana na kutoa mapendekezo kwa viongozi wa mkutano wa WEF juu ya nini kifanyike ili kuona jamii ya Waafrika inanufaika na uwekezaji pamoja na kuwa na usawa katika ukuaji wa uchumi.
  Bi. Kiangi alisema ni dhahiri kwamba kumekuwa na ukuaji wa uchumi kwa nchi za Afrika lakini wanaonufaika na ukuaji wa uchumi huo ni wachache na hivyo ni muhimu kujiuliza
ni nani ananufaika na uchumi huo.

0 comments:

Post a Comment