SONYA_FLAWLESS_IMG
WE CREATE GREATNESS. | Professional Networker | Global Business Builder | Health And Wellness Coach | YOUR DREAM OUR PLAN.

Tuesday, May 4, 2010

Dar es S alaam kuzizima kwa ugeni mkubwa

JIJI la Dar es Salaam leo linaanza kuzizima kutokana na ugeni wa watu zaidi ya 1,000 kutoka nchi 85 wanaowasili kushiriki mkutano wa Uchumi wa Dunia kuhusu Bara la Afrika (WEF).

Jamii ya wakazi wa Dar es Salaam imekuwa katika nafasi ya kuufahamu mkutano huo, hususan baada ya kutangazwa uamuzi wa kufunga baadhi ya barabara kwa ajili ya kupisha shughuli za mkutano huo ambao umetajwa kuwa na manufaa makubwa kwa nchi.

Tangu ilipotangazwa juzi kwenye televisheni juu ya uamuzi wa kufunga kwa muda baadhi ya barabara, zimekuwapo hoja kutoka watu mbalimbali juu ya kile kinachoelezwa, kwamba hatua hiyo itaongeza msongamano wa magari katika Jiji.

Hata hivyo akizungumza jana na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, aliwaondolea wasiwasi wakazi hao kwamba barabara hizo hazitafungwa moja kwa moja isipokuwa katika muda maalumu.

Lukuvi alisema hata wakati wa msafara, magari ya dharura yakiwamo ya zimamoto na ya wagonjwa yataruhusiwa kupita. Alisema pia magari ya wanafunzi na wafanyakazi yataruhusiwa kupita wakati utakapopatikana upenyo.

Kwa mujibu wa Lukuvi, barabara hizo zitaanza kufungwa kuanzia leo hadi Jumamosi; mkutano utakapofungwa.

“Barabara hizi zilizoteuliwa, zitakuwa zinafungwa na kufunguliwa mpaka mkutano uishe na hii itasimamiwa na polisi wetu, hivyo wananchi watarajie usumbufu kidogo,” alisema.

Barabara zitakazofungwa ni ya Nyerere kutoka Uwanja wa Ndege hadi katikati ya Jiji ambayo itatumiwa na wageni wanaokuja kuhudhuria mkutano huo unaofunguliwa rasmi kesho.

Kesho hadi Ijumaa, kuanzia saa moja mpaka saa tatu asubuhi, barabara ya Ali Hassan Mwinyi itatumika kusafirisha wageni kwenda kwenye kumbi za mikutano zilizopo kando ya barabara ya Sam Nujoma.

Mkuu wa Mkoa alifafanua, kwamba barabara hizo zitafungwa kutokana na wageni wengi kulala katika hoteli zilizo katikati ya Jiji na kwamba baadaye zitafunguliwa kwa matumizi ya kawaida.

Itakapofika saa 9 alasiri, barabra hizo zitafungwa tena hadi saa moja usiku kwa ajili ya washiriki wa mkutano kurudi katika hoteli walimofikia.

Wakazi wa Sinza, Kijitonyama, Mwenge na wote wanaotumia barabara ya Ali Hassan Mwinyi, wanashauriwa kutumia barabara ya Morogoro huku wakazi wa Mbezi, Mikocheni, Kawe, Msasani wameshauriwa kutumia barabara ya Old Bagamoyo ili kuepuka usumbufu.

Aidha, wananchi wanaopata huduma katika maduka ya Mlimani City wameshauriwa kutumia barabara ya Chuo Kikuu cha Ardhi, kwani barabara ya Sam Nujoma, itakuwa ikitumika kwa shughuli za mkutano huo.

Hata hivyo, Lukuvi aliomba radhi wananchi kwa usumbufu utakaojitokeza kwa kipindi chote cha mkutano huo ambao unatarajiwa kuinufaisha nchi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa WEF, tangu taasisi yake ianze kuandaa mikutano ya aina hii, haijawahi kupata washiriki wengi kama ilivyo katika mkutano huu unaofanyika nchini.

Katika hatua nyingine, wanaharakati kutoka zaidi ya nchi 10 za Afrika, wamejiandaa kuandamana katika barabara ya Sam Nujoma.

Katika barabara hiyo, ndiko uliko ukumbi wa Mlimani City, ambako mkutano huo utafanyika, na wanaharakati hao wana lengo la kuwasisitiza viongozi wa nchi mbalimbali kukumbuka majukumu yao ya kupambana na matatizo yakiwamo ya kiafya.

Taarifa ya Jonathan Rousse, ambaye ni Mkuu wa Idara ya Uhusiano wa Jamii, Masoko na Maendeleo wa Umoja wa Watetezi wa Haki na Mapambano dhidi ya Ukimwi Afrika Kusini (Arasa), ilisema maandamano hayo yatafanyika kuanzia saa 4 asubuhi.

Katika mkutano kama huo uliofanyika Cape Town, Afrika Kusini mwaka jana, wanaharakati hao waliandamana huku wakibeba puto mfano wa jicho likiwa limeandikwa ‘We Are Watching – Fund the fight against HIV and TB (Tunaona – Fadhilini mapambano dhidi ya virusi vya Ukimwi na Kifua Kikuu)’.

Lengo lilikuwa ni kuwakumbusha viongozi wa Dunia ahadi zao za kufadhili na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya katika kuzuia maambukizi ya virusi, tiba na huduma.

Maandamano ya mwaka huu kwa mujibu wa Rousse, ni kuwakumbusha viongozi hao jinsi walivyoshindwa kutekeleza ahadi zao katika kuhakikisha huduma hiyo inapatikana, kwani hali hiyo imekuwa pigo kwa Waafrika, kwani uchumi wa nchi zao hauwezi kukua kama wananchi hawana huduma nzuri za kiafya.

“Mamia wanatarajiwa kushiriki maandamano haya, wakiwa wamebeba maputo mithili ya macho, ili kuwakumbusha viongozi kwamba tunaona na tunapanga kuwawajibisha kutokana na ahadi zao katika sekta ya afya,” alisema Rousse katika taarifa yake.

Alisema risala inayozungumzia malalamiko ya jamii, itawasilishwa kwa Mkurugenzi wa Uhusiano wa Nje wa Mfuko wa Kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria, pia Kamishna wa Afya wa Serikali ya Tanzania, ambaye atasambaza ujumbe huu kwenye mkutano huo wa uchumi.

0 comments:

Post a Comment